Back to top

Mahakama ya Kisutu yatoa hukumu kesi ya Maxence Melo wa Jamii Forums.

17 November 2020
Share

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemhukumu kifungo cha nje Mkurugenzi Mtendaji wa Jamii Media, Maxence Melo baada ya kumtia hatiani  kwa kosa la kuzuia askari kutekeleza majukumu yao, kwa masharti ya kutokurudia kosa hilo ndani ya mwaka mmoja.

Hukumu hiyo ilisomwa mahakamani hapo na Hakimu Mkazi mkuu, Huruma Shaidi huku upande wa mashtaka ukiwakilishwa na wakili wa serikali Faraji Ngukah.

Mahakama hiyo imemwachia huru mshtakiwa namba mbili katika kesi hiyo, Mike Mushi baada ya kukuta hana hatia katika makosa yote yaliyokuwa yakiwakabili ambapo Hakimu Shaidi amesema Mushi alikuwa ni kama msindikizaji katika kesi hiyo.

Hukumu hiyo ilitolewa baada ya upande wa mashtaka kufunga ushahidi wao kwa kuleta mashahidi sita huku Melo akijitetea mwenyewe bila kuwa na shahidi mwingine.

Awali,  Wakili wa Serikaki Faraji Ngukah ameiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali kwa mshitakiwa kwani kitendo alichokifanya cha kuzuia askari kutekeleza majukumu yao ni hatari kwa taifa.