Back to top

Mahakama yamwachia huru aliyekuwa Mwendesha Mashtaka.

18 October 2021
Share

Mahakama ya Hakimu Mkazi  Manyara imemwachia huru aliyekuwa mwendesha mashtaka wa mkoa wa Manyara Mutalemwa Kishenyi aliyekuwa akikabiliwa na tuhuma za kuomba na kupokea rushwa ya shilingi milioni tano baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha mahakamani.


Akitoa hukumu hiyo Hakimu Elimo Daniel Massawe amesema kuwa mahakama imepitia ushahidi wa pande zote mbili na kuona kuwa mwendesha mashtaka huyo hana hatia kama ilivyodaiwa awali kuwa alipokea rushwa kutoka kwa mfanyabiashara Gasper Mlay kwa lengo la kumsaidia mfanyabiashara huyo ambaye aliwahi kuwa moja kati ya  wakurugenzi wa kampuni inayozalisha vinywaji vikali mkoani humo iliyokuwa ikakabiliwa na mashauri ya masuala ya kodi.


Aidha  Hakimu amesema kuwa  TAKUKURU walipochukua vielelezo kama pesa na simu havikusainiwa na mashahidi katika eneo la tukio kwa mujibu wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na rushwa na badala yake vilisainiwa katika Ofisi za TAKUKURU mkoa hivyo vieleelezo hivyo havifai kutumika mahakamani.

Pia Mahakama imethibitisha kuwa shahidi wa upande wa mashtaka Gasper Mlay hakuwa  mfanyakazi wa Kampuni ya Mati Super Brands hivyo hakutumwa na mkurugenzi wa kampuni hiyo David Mulokozi kupeleka rushwa ya milioni tano kwa aliyekuwa mwendesha mashtaka wa serikali Mutalemwa. 

Hakimu amesema kuwa mahakama imeona kuwa kuna mashaka mazito na mengi kwa upande wa mashtaka kushindwa kuthitisha kuwa Mutalemwa ana makosa hivyo mahakama imeamua kumwachia huru.