Back to top

Majaliwa amsimamisha Kazi Afisa Mipango wa H/Wilaya ya Liwale.

08 October 2021
Share

Waziri Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Afisa Mipango wa Halmashauri ya Wilaya ya Liwale Bw.Omary Chingwile ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za matumizi mabaya ya fedha za ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Liwale na kuviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi juu ya tuhuma hizo.

"Hatuwezi kufanya mchezo na fedha ya Serikali, tunahitaji kila mradi uende vizuri, fedha iliyoletwa lazima itumike kama ilivyokusudiwa".

Mhe.Majaliwa amesema Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan amesisitiza matumizi mazuri ya fedha za umma ili zikamilishe miradi ya maendeleo ya wananchi na kwamba Serikali haitamvumilia mtumishi yoyote anayetumia vibaya fedha za umma.

Waziri Mkuu amemsimamisha kazi mtumishi huyo wakati akizungumza na madiwani, watumishi na wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Liwale akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo katika Mkoa wa Lindi.