Back to top

MAJALIWA ATOA MAAGIZO KWA UONGOZI WA JIJI LA DODOMA

25 November 2022
Share

Waziri Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa, ameuagiza uongozi wa Jiji la Dodoma, ushirikiane na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini ili kutengeneza mpangilio safari za daladala ndani ya jiji hilo kuelekea soko jipya la wajasiriamali wadogo lililoko barabara ya Bahi.

Aidha ameutaka Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini -TARURA mkoa wa Dodoma ukiboreshe kituo cha mabasi kilichoko eneo hilo ili kiweze kukidhi viwango vya kupokea magari ya abiria yatakayo elekezwa eneo hilo.

Ametoa maagizo hayo baada ya kukagua soko jipya la wajasiriamali, wadogo lililoko Bahi Road Jijini Dodoma.

Mhe.Majaliwa pia ameitaka Halmashauri ya Jiji la Dodoma, isimamie utoaji wa fedha za mikopo kwa wafanyabiashara katika soko hilo, ili waongeze mitaji na kukuza biashara zao.

Amesema ni dhamira ya dhati ya kuendelea kuwainua wafanyabiashara kwa kufungua milango ya ufanyaji biashara kwa uwazi na Serikali kuwapa huduma muhimu zitakazowasaidia kuleta tija kwenye shughuli zao.