Back to top

Majaliwa: TAKUKURU hakikisheni Watanzania hawarubuniwi.  

12 August 2020
Share

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ihakikishe Watanzania hawarubuniwi ili watumie vizuri utashi wao wa kisiasa kuchagua viongozi bora.

Ametoa agizo hilo Agosti 12, 2020 alipofungua jengo la Intelijensia TAKUKURU Makao Makuu Dodoma. Amewasihi watumie vizuri ofisi hiyo kukusanya taarifa muhimu za kiintelijensia zinazowahusu wagombea, vyama au wananchi watakaojihusisha na vitendo vya rushwa kwenye Uchaguzi Mkuu.

Waziri Mkuu amesema wananchi wanatakiwa kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura Oktoba 28, 2020 na kwamba wanawajibu wa kuchagua Serikali bora na kiongozi bora atakayewaletea maendelea maendeleo. “Chagueni kiongozi mwenye maono aliyetenda na atakayetenda.”

Waziri Mkuu amesema wanapoelekea kwenye Uchaguzi Mkuu, ni vema Watanzania wote na viongozi wakazingatia nasaha za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, katika moja ya hotuba zake alipowataka wajiulize kwamba mgombea anayetumia rushwa kununua kura amepata wapi fedha hizo na je, akipata uongozi, fedha hizo atazirudishaje.

 “Kwa hivyo, nasi ifike mahala tuwahoji hawa wanaotutia doa. Je, wewe mwenzetu unayetumia rushwa kununua uongozi umepata wapi fedha hizo? Na je? tukikuchagua, utarejesha vipi fedha hizo? Nitoe wito kwa Watanzania wote, msikubali kuwachagua wagombea wanaotumia rushwa ili kupata nafasi za uongozi.”.Majaliwa.