
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, amesema Serikali kwa sasa inaimarisha mifumo itakayozuia wanyamapori wakiwemo tembo, kuingia katika makazi ya wananchi ili waweze kuishi kwa amani.
Ameyasema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Mlalo Rashidi Shangazi, katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu, Bungeni jijini Dodoma.
Amesema baada ya Serikali kuimarisha ulinzi na kuzuia uwindaji haramu, kwa sasa nchini kuna ongezeko kubwa la wanyama, hivyo inafanya jitihada kuzuia wanyama hao kuingia katika makazi.
Mbunge huyo alihoji ni kwa kiasi gani Serikali itawahakikishia wananchi wanaoishi pembezoni mwa hifadhi hizo, usalama wao ili wasiendelee kupata athari kutokana na uvamizi wa wanyama hao.
Amesema jitihada zingine ni pamoja na kuimarisha na kujenga vituo vya kuhifadhia silaha, ili kusaidia kuwaondoa wanyama hao na kuwarudisha katika maeneo yao ya hifadhi.
Waziri Mkuu amesema kwa sasa Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii inaratibu ujenzi wa vituo 32, vya kuhifadhia silaha kandokando ya maeneo yanayopakana na hifadhi za wanyamapori.
