Back to top

Majambazi 3 wauawa katika majibizano ya risasi na polisi Mwanza.

09 March 2019
Share

Watu watatu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi wameuawa kwa kupigwa risasi na askari polisi katika maeneo ya Murungushi Igogo jijini mwanza wakati wakijaribu kurushiana risasi na askari polisi waliokua doria jirani na ghala la kiwanda cha Avant linalotumika kuhifadhi bidhaa za vipuli vya magari na vifaa vya ujenzi, huku majambazi wengine wakifanikiwa kukimbia baada ya kukaidi amri ya kujisalimisha.

Kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza Kamishna msaidizi wa polisi Muliro Jumanne Muliro amesema majambazi hao waliouawa walikuwa na silaha aina ya shortgun iliyokuwa na risasi 4, mapanga matatu, nondo moja, mkasi mkubwa wa kuvunjia milango na makufuli na pia funguo nyingi zinazotumika kufungulia milango, makufuli na droo za ofisi na maghala.

Kwa mujibu wa Kamanda Muliro, majambazi hao waliofariki wana umri kati ya miaka 30 hadi 35 na miili yao imehifadhiwa katika hospitali ya mkoa wa Mwanza Sekou Toure kwa uchunguzi na utambuzi zaidi, ambapo watuhumiwa wengine wa ujambazi waliotoroka eneo la tukio wanasakwa kwa udi na uvumba ili watiwe nguvuni na jeshi la polisi.