
Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameelekeza majeruhi wote wa ajali iliyotokea Meatu Mkoani Simiyu, ikiwa ni katika ziara yake mkoani humo watibiwe kwa gharama za Serikali.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama leo, alipotekeleza agizo la Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan la kutembelea na kujua hali za majeruhi hao watano (5) wanaoendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda BUGANDO Mkoani Mwanza.
"Mhe. Rais amenituma, amesema haiwezekani kama Serikali kuendelea tu na ziara wakati Watanzania wamepata matatizo, ndio maana nimekuja, na wagonjwa hawa wote watalipiwa gharama na Serikali, na hii ndio aina ya Rais ambaye tuko naye anayejali afya na utu wa wananchi wake," Amesema Waziri Mhagama
Aidha, Waziri Mhagama ametembelea wodi ya watoto pamoja na wazazi katika hospitali hiyo kwa lengo la kuangalia na kukagua huduma zinavyotolewa ambapo kwa ujumla ameridhishwa na huduma hizo zinazotolewa na madaktari bingwa na bobezi.
"Lakini pia, leo nimekuja kushuhudia wanafunzi Kumi wa darasa la uuguzi wabobezi wanofanya vizuri katika utoaji wa huduma za kibingwa kwenye ngazi ya watoto ambao wametokana na 'Samia Schoraship Fund' ambao wametoa pongezi na shukurani kwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan," amesema Waziri Mhagama.
Amesema, Serikali kwa sasa imeweka utaratibu wa kusomesha kwa seti wataalam mbalimbali wakiwemo wauguzi ili kukidhi kiu, mahitaji na maono ya Mhe. Rais Dkt. Samia pamoja na kupanua wigo wa tiba utalii, kupunguza vifo vya kina mama na watoto.
Pia, ameipongeza Hospitali hiyo kwa kutoa huduma bora kwa kushirikiana na Serikali kwa kuwa Sekta ya Afya ni washirika wa sekta binafsi.
Amesema, Hospitali hiyo ni muhimu sana kwakuwa inatoa huduma za ubingwa na ubingwa bobezi ambayo inapokea wagonjwa zaidi ya 1600 kutoka katika mikoa nane(8) ikiwemo mkoa wa Simiyu.
Waziri Mhagama ameutaka uongozi wa hospitali hiyo kufanyia kazi maeneo yanayohitaji maboresho na kuhakikisha kila aina ya uwekezaji uliofanywa unatunzwa.