Back to top

"MAJONGOO BAHARI, MWANI, KAA NI BIASHARA KUBWA"-ULEGA

15 January 2024
Share


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe.Abdallah Ulega, amewahimiza wananchi wanaoishi Mtwara na maeneo mengine ya ukanda wa Pwani ya Bahari ya Hindi, kuchangamkia fursa ya ufugaji wa Majongoo Bahari, Kaa, Kambakochi pamoja na kufanya kilimo cha Mwani kwa sababu mazao hayo yanahitajika sana katika nchi za Asia hususan China.

Waziri Ulega ametoa rai wakati wa ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa Kituo cha Ukuzaji Viumbe Maji cha Ruvula kinachojengwa Msimbati, mkoani Mtwara.

Halikadhalika, amewahimiza wananchi kujipanga vyema ikiwemo kuunda vikundi ili serikali iweze kuwatambua na kuwapatia mikopo ya vifaa vya kisasa kwa ajili ya kuwawezesha kufanya shughuli zao kwa ufanisi mkubwa.

Aidha, Waziri Ulega ameonesha kuridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho cha ukuzaji viumbe maji cha Ruvula huku akiamini kuwa kitakamilika kwa wakati ili kianze kufanya kazi.

Awali, Mhandisi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bw. George Kwandu alimweleza Waziri Ulega kuwa ujenzi wa kituo hicho umefikia asilimia 90 na kwamba mpaka itakapofika Januari 30, 2024 mradi huo utakuwa tayari umekamilika.