Back to top

Makamu wa Rais awaasa mabalozi kuweka maslahi ya Tanzania mbele.

01 October 2021
Share

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango amewaasa mabalozi kuweka maslahi ya Tanzania mbele wakati wote watakapokuwa wakiiwakilisha nchi na kufanya kazi kwa bidii na weledi ili kukuza ushirikiano wenye manufaa baina ya Tanzania na maeneo yao ya uwakilishi hasa kwa kuweka mkazo katika Diplomasia ya Kiuchumi.

Ameyasema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na waheshimiwa Mabalozi watakaoiwakilisha Tanzania katika nchi za Rwanda, Sweden, Uturuki, Korea Kusini, Uswisi, India na Ethiopia mazungumzo yaliofanyika Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma walipofika kumuaga kabla ya kuelekea kwenye vituo vyao vipya vya kazi.

Amesema ni vema mabalozi hao kwenda kujifunza yale ambayo yanafanyika katika nchi hizo na kuhamisha maarifa hayo kwa lengo la kukuza na kuendeleza uchumi wa Tanzania. 

Makamu wa Rais amesema zipo nchi zilizoendela katika sekta ya utalii hivyo mabalozi hawana budi kujifunza na baadae kuvutia watalii hao kufika Tanzania kwa manufaa ya nchi. Aidha amewaagiza mabalozi hao kuanzisha na kuimarisha ushirikiano wa kibiashara ikiwa pamoja na kutafuta masoko kwa ajili ya bidhaa za Tanzania.

Akizungumza kwa niaba ya mabalozi hao Balozi wa Tanzania nchini Uturuki Mhe. Luteni Jenerali Yakub Mohamed amesema wapokea miongozo yote waliopewa na Makamu wa Rais na hivyo kuahidi kwenda kuiwakilisha vema Tanzania katika vituo vyao.