
Makandarasi wazawa wameaswa kuzisimamia kampuni zao kwa kufuata mfumo wa kisheria na udhibiti, lengo ni kutaka kazi zao zisimamiwe kwa kufuata vipengele vya ubia sambamba na sheria ya manunuzi ya umma na ulipaji kodi kwa wakati.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Idara ya Utafiti na Maendeleo kwa Makandarasi, Mhe. David Jere katika mafunzo ya siku mbili kwa Makandarasi mkoani Mtwara.

Jere amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo makandarasi wa namna nzuri ya kuunda ubia wenye mafanikio katika matumizi ya mfumo mpya wa manunuzi kwa Umma kwa njia ya mtandao (NeST) na elimu ya kodi katika miradi ya ubia.
Amesema kwa kufanya hivyo, kutawajengea weledi wa kutumia wataalamu stahiki katika sekta mbalimbali ili kukwepa changamoto kwenye maeneo yao ya kazi.
Amesema anaamini makandarasi waliowahi kutekeleza miradi hiyo wamepata ujuzi mkubwa.
Hata hivyo, alisisitiza makandarasi washiriki mafunzo mbali mbali yanayoandaliwa na CRB ili kuwaongezea thamani kwa kuwa ujuzi unaongeza ufanisi kwenye shughuli yoyote ile.
Awali, Mkurugenzi wa kampuni ya Abbey Engineering ya Ndanda mkoani Mtwara, Mhe. Kazungu Magili, aliishukuru Bodi kwa kuratibu mafunzo hayo ambayo yamewajengea uwezo wa namna ya kuandaa mikataba ya ubia.
Alisema awali wengi wao walianzisha kwa mihemuko na kujikuta wakiingia kwenye migorogoro.
Naye Mhe. Leonard Mangu, Mkurugenzi wa Oxo Africa Company Limited ya Dar es salaam, alisema mafunzo hayo yameewajengea uwezo wa jinsi ya kutatua changamoto mbali mbali kupitia michango kutoka kwa Makandarasi waliowahi kutekeleza miradi ya ubia na kupitia midahalo iliyokua inafanyika na kuahidi Bodi kuwa yote waliyojifunza wataenda kuyafanyia kazi kwa vitendo.
Aidha Mhe. Isaac Nguga, Mkurugenzi wa biashara wa Oxo Africa Company Limited wa Dar es Salaam, alisema mafunzo haya yamewajengea uwezo wa kuzingatia sheria na udhibiti wa kusimamia mikataba ya ubia na kutoa rai kwa Serikali kuwa miradi mikubwa inayoendelea kutekelezwa nchini hivi sasa izingatie na makandarasi wa ndani.
