
Makandarasi wazawa wametakiwa kuzisimamia kampuni zao kwa ufasaha kwa kufuata sheria za ulipaji wa kodi kwa wakati, na kufanya kazi kwa weledi kwa kutumia wataalamu stahiki katika sekta mbalimbali ili kukwepa changamoto katika maeneo yao ya kazi.
Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo yenye lengo la kuwajengea uwezo Makandarasi wazawa kibiashara, Jijini Dodoma, Msajili wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), Mhe.Rhoben Nkori, amesema kuwa lengo moja wapo la kufanya mafunzo hayo ni pamoja na kutoa elimu kwa makandarasi kuhusiana na mvutano baina yao na mamlaka ya mapato Tanzania (TRA).
Mhe.Nkori, amesema makampuni mengine hutumika kufanya kazi kwa majina ya wamiliki wengine yanayopelekea mvutano pindi kazi inapoenda kukaguliwa na TRA kupitia Bodi ya Usajili wa Makandarasi(CRB) hivyo amewataka wamiliki wa makampuni kusimamia vyema makampuni yao ili kuepuka changamoto hizo.
Mha.Nkori amesisitiza kuwa ili kuendelea kujenga taswira nzuri kwa makandarasi nchini, Bodi itaendelea kuwachukulia hatua kisheria makandarasi wote wanaokiuka maadili yao ya kazi.
Aidha ametoa wito kwa Makandarasi wa ndani kusimamia kwa weledi kampuni zao kwa kutumia wataalamu stahiki na kutekeleza miradi kwa viwango vyenye ubora wa hali ya juu ili watanzania waweze kunufaika na miradi hiyo.
Mafunzo hayo ya siku tatu yanayotolewa na Bodi yameshirikisha Makandarasi kutoka sehemu mbalimbali nchini lengo likiwa ni kubadilishana uzoefu na kuwajengea uwezo makandarasi hao katika mujukumu yao ya kazi.
