Back to top

Makontena 187 ya vinia yapata kibali kwenda nje.

24 November 2021
Share

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro ameruhusu kusafirisha makontena 187 ya Vinia kwenda nchi za nje  yaliyokuwa yamekwama  bandarini baada ya kutoa tamko la  kuzuia usafirshaji malighafi za mazao ya misitu kwenda nchi za nje  ikiwemo vinia.


Waziri Dkt. Ndumbaro ametoa ruhusa hiyo leo wakati alipokuwa akizungumza na k Wafanyabishara wa mazao ya misitu katika mkutano ulioitishwa na Wafanyabiashara hao Jijini Dar es Salaam kupitia Baraza la Taifa la Wafanyabishara (TNBC) wakiomba kuongezewa muda wa kusafirisha mazao hayo. 

Hatua hiyo inakuja kufuatia ombi la Wafanyabishara wa mazao ya misitu wakimtaka  aongeze muda wa kusafirisha mazao ya misitu kwenda nchi za nje baada ya  kupigwa  marufuku kuanzia Novemba 15 mwaka huu.akiwa mkoani Iringa.

Licha ya kuruhusu usafirishaji wa  makontena hayo 187 yaliyokuwa na vinia, Dkt. Ndumbaro ameendelea kushikilia msimamo wake wa kutoruhusu uvunaji na biashara ya gundi ndani na nje ya nchi mpaka pale watafiti watakapotoa hasara na faida yake.

Vinia ni Malighafi iliyochakatwa nusu kutoka kwenye gogo ambalo Wawekezaji wengi husafirisha nje ya nchi kwa ajili ya kutengeneza bidhaa mbalimbali hususan mbao laini (plywood) ambazo hurejeshwa tena nchini kuuzwa kwa bei ya juu.