
Wizara ya Maliasili na Utalii inaendeleza jitihada za kuhifadhi vyema maeneo yenye historia adhimu nchini yakiwemo majengo na mahandaki yaliyotumiwa na wapigania uhuru kutoka nchi za Kusini mwa Afrika Wilayani Kongwa Mkoani Dodoma, ili yaweze kuongeza tija katika sekta ya Utalii.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Mambo ya Kale, kwenye Mbio za hiyari zijulikanazo kama Kongwa: African Liberation Marathon, Mhifadhi Mkuu Idara ya Malikale Bi. Prisca Kirway amesema Wilaya ya Kongwa ina utajiri mkubwa wa Malikale ambao ni kielelezo muhimu cha Kitaifa na Kimataifa.
“Kama Wizara, eneo hili la Kongwa ni muhimu sana kwa kutunza urithi wa Kihistoria na Utalii, Hivyo kwa umuhimu huo Wizara imefanya jitihada za kuhakikisha eneo hili linaingia katika Orodha ya Maeneo ya Urithi wa Taifa kwa kupewa Tangazo la Serikali- GN ili lilindwe na kuhifadhiwa kisheria”. Alisema Bi Kirway.

Akizungumzia Mbio hizo, Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Remidius Mwema, amesema, lengo la mbio hizo ni kuijulisha Dunia na kurithisha kizazi kilichopo, kupitia Michezo Historia ya mchango mkubwa wa Tanzania katika ukombozi wa Bara la Afrika kupitia Wilaya ya Kongwa.
