Back to top

Malori zaidi ya 30 yaliyobeba madini ujenzi yazuiliwa mkoani Mwanza

18 September 2019
Share

Malori zaidi ya 30 yaliyokuwa yamebeba madini ujenzi kutoka wilaya ya misungwi kwenda jijini mwanza, yamezuiwa katika eneo la buhongwa wilayani nyamagana kuendelea na safari kwa takribani saa nane baada ya madereva wa malori hayo kugoma kulipa ushuru wa kuingiza malighafi hiyo jijini humo kwa madai kuwa ni kinyume cha sheria.

Mwenyekiti wa chama cha madereva wa malori aina ya 'Tipper' yanayofanya shughuli za usafirishaji wa mchanga na aina nyingine za madini ujenzi katika wilaya ya Nyamagana Paschal Kashiga anaeleza sababu zilizosababisha malori hayo kukamatwa na askari mgambo wa jiji.

Baadhi ya madereva wa malori jijini Mwanza wameiomba serikali kuu kuingilia kati mgogoro huo kufuatia halmashauri ya jiji la Mwanza kudaiwa kuwatoza ushuru mara mbili, licha ya baadhi yao kulipia katika halmashauri ya Misungwi kiasi cha shilingi 3,000, pamoja na shilingi 2600 kama kodi ya wakala wa madini.

Wakala wa ushuru wa madini ujenzi katika halmashauri ya jiji la Mwanza Nurdin Kangezi anasema utaratibu huo wa kutoza ushuru wa kuingiza mchanga na kokoto katika jiji la Mwanza unafahamika kwa muda mrefu, hivyo amewaomba kufuata kanuni na sheria badala ya kufanya mgomo.

Tangu serikali ifanye marekebisho ya sheria ya madini ya mwaka 2010 na kupitisha marekebisho ya sheria ya madini ya mwaka 2017, utekelezaji wa sheria hiyo umekuwa na changamoto kadhaa kutoka kwa baadhi ya wadau, wakiwemo wa sekta ya madini ujenzi na viwandani ambapo elimu zaidi inatakiwa kuendelea kutolewa kwa wadau.