
Kampuni ya Marvel Studios, imeamua kuachana na mwigizaji Jonathan Majors, baada ya kukutwa na hatia ya kumpiga na kumnyanyasa mpenzi wake wa zamani.
Majors (34) nyota wa Ulimwengu wa Sinema, alijulikana sana kupitia tamthilia (series) Loki, na Ant-Man And The Wasp: Quantumania.
Majors alipangwa kuwa muigizaji mkuu kwenye filamu inayofuata ya Avengers inayotazamiwa kutoka May 1, 2026, lakini kufuatia tukio hilo hatoonekana tena.
Lakini pia Msemaji wa studio ya filamu, inayomilikiwa na Disney alisema mwigizaji huyo hataonekana tena kwenye filamu zijazo zitakazozalishwa na kampuni hiyo.
Mashtaka dhidi ya mwigizaji huyo, yalitokana na mzozo kati yake na mpenzi wake wa zamani wa Uingereza, Grace Jabbari, ulioanzia kwenye kiti cha nyuma cha gari huko New York City.
Jabbari, mchezaji densi mwenye umri wa miaka 30, alimtuhumu Majors kwa kumsababishia maumivu makali, kufuatia shambulio hilo la ndani ya gari.
Alisema alimpiga kichwani, akasokota mkono wake nyuma ya mgongo wake na kuminya kidole chake cha kati hadi kikavunjika.
Kwa upande wa Mawakili wa Majors walisema kuwa Mwanamke huyo ndiye mchokozi, wakidai kuwa alipandwa na hasira baada ya kusoma ujumbe mfupi wa maandishi kwenye simu ya Majors uliotumwa na mwanamke mwingine na huwenda ni mpango wa kumchafua Majors.
