Back to top

MASAUNI :MKAWE MFANO BORA KWA ASKARI WENGINE.

25 March 2024
Share

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhandisi Hamadi Masauni amewataka askari waliohitimu mafunzo ya awali ya askari polisi katika kambi ya kilele Pori wilayani Siha mkoani Kilimanjaro, kwenda kutoa huduma bora kwa wananchi , huku akiwataka kuwa mfano kwa askari watakaowakuta katika mikoa na vituo vya kazi watapopangiwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi wanakokwenda.

Waziri Masauni amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk.Samia Suluhu Hassan, kwa namna ambavyo ameviwezesha vyombo vya ulinzi katika kuongeza idadi ya askari, ambao wanakwenda kuimarisha ulinzi na usalama wa Tanzania.

Kwa upande wa Kamishna wa Polisi Fedha na Logistiki CP Liberatus Sabas ambaye amemwakilisha Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini amewataka askari hao wapya kutambua kuwa askari ni kioo cha  Jamii ambapo amewataka kwenda kutatua changamoto za wananchi wanaolitegemea Jeshi hilo.

Kamishna wa Polisi Operesheni mafunzo wa Jeshi la Polisi CP Awadhi Juma Haji amebainisha kuwa mafunzo ya kijeshi yanahitaji uvumilivu na nidhamu kubwa ili uweze kufaulu mafunzo hayo ambapo amesema wataendelea kuwafundisha askari hao wakiwa kazini ili kuwajengea uwezo wa kiutendaji.

Mkuu wa Shule ya Polisi Tanzania Kamishna msaidizi mwandamizi wa Polisi SACP Ramadhan Mungi amesema askari hao wamefundishwa mambo mengi ambayo yamewajenga kitaluma na kijeshi huku akibainisha kuwa wapo wanafunzi ambao wamefukuzwa mafunzo kwa kutokizi viwango vya Jeshi hilo ambao Jumla yao ni 193.