Back to top

Mashine za kuchanganya chumvi na madini joto zakabidhiwa.

24 February 2022
Share

Wizara ya Afya imekabidhi mashine tano za kisasa za kuchanganya chumvi na madini joto kwa Ofisi ya Rais TAMISEMI zilizotolewa na Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania kupitia Shirika la Kimataifa la Nutrition International kwa ajili ya kusimikwa katika Mikoa ya Tanga, Pwani na Mtwara itayosaidia kuongeza uzalishaji wa chumvi yenye kiwango cha  kutosha cha madini joto nchini.


Akizungumza wakati wa kukabidhi mashine hizo kwa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI, Katibu Mkuu Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi amesema Utafiti uliofanyika nchini mwaka 2019 ulibaini Tanzania inazalisha chumvi Tani 330,712 kwa mwaka na kati ya chumvi hiyo tani 141,228 ambapo ni sawa na asilimia 43 haiwekwi madini joto hivyo ujio wa mashine hizo utasaidia kuongeza uzalishaji wa chumvi yenye madini hayo.


Prof Makubi amesema mashine hizo ambazo zimetengenezwa nchini na Wataalamu kutoka VETA zimeweza kugharimu kiasi cha shilingi milioni 55 huku gharama ya mashine moja ikigharamu kiasi cha shilingi milioni 11 na kusaidia kuokoa milioni 14 kwa kila mashine endapo zingeagizwa kutoka nje ya nchi.


Awali akitoa maelezo juu ya programu ya kuzuia upungufu wa madini joto nchini Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania Dkt. Germana Leyna amesema madini joto ni moja ya kirutubisho muhimu kwa ukuaji mzuri wa akili na mwili wa binadamu na endapo mtu atakuwa na upungufu wa madini joto basi anaweza kupata madhara mbalimbali ikiwa ni pamoja na udumavu wa akili na mwili.


Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Nutrition International Dkt. Daniel Nyagawa amesema katika Mpango mkakati wake wa miaka 6 ulioanza mwaka 2018 hadi 2024 shirika hilo limejielekeza kufanya kazi zake kwa karibu na Serikali na taasisi zake ili kwa pamoja  kuweza kupambana na utapiamlo na madhara yatokanayo na utapiamlo.


Akizungumza kwa niaba ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Katibu Mkuu Prof. Riziki Shemdoe ameipongeza VETA kwa kuanza kutengeza mashine hizo kwa gharama nafuu tofauti na zingeagizwa toka nje ya nchi na amewaagiza makatibu tawala wa mikoa itakayopewa mashine hizo kuhakikisha  wanazitumia ipasavyo na siyo kwenda na kuzifungia stoo.