
Jeshi la Polisi Tanzania, linapenda kutoa tahadhari kwa wananchi kuwa makini na baadhi ya watu au vikundi vya watu wanaowatapeli wananchi kwa kuwapigia simu au kuwatumia ujumbe wa maneno, huku wakijitambulisha kwa majina ya viongozi wa wizara, au taasisi fulani na kwamba wana kampeni au wanachangisha fedha kwa ajili ya kitu fulani.
Jeshi hilo pia limetoa wito kwa Mwananchi yeyote, atakayepigiwa simu au kutumiwa ujumbe wa maneno na watu wa aina hiyo, atoe taarifa katika kituo cha Polisi kilicho karibu au atume namba hiyo ya utapeli kwenda namba 15040, huku wakiwataka kuepuka kufuata maelekezo kutoka kwa mtu au watu wa aina hiyo, ikiwemo maelekezo ya kufanya miamala ya kifedha.
Aidha, Jeshi la Polisi linaendelea kufanya uchunguzi, ili kuendelea kuwabaini na kuwakamata wale wote wanaojihusisha na vitendo hivyo, vya kihalifu ili kuwachukulia hatua za kisheria.
Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi, kwa kutoa taarifa za wahalifu na uhalifu ikiwemo uhalifu, kwa njia ya mitandao mara tu wanapoona viashiria, ili hatua za haraka ziweze kuchukuliwa dhidi yao.
