
Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Lindi, umefanikiwa kurejesha mawasiliano yaliyokuwa yamekatika kati ya Kilwa Masoko- Nangurukuru wilaya ya Kilwa na wilaya ya Liwale mkoani Lindi kufuatia mvua kubwa zilizoambatana na upepo hivi karibuni.
Mawasiliano hayo yamereshwa, kupitia kazi iliyofanyika usiku na mchana, ya kuhakikisha daraja la muda katika Mto Zinga, ambao unatenganisha kijiji cha Zinga na Miguruwe, linatengamaa ili shughuli za usafirishaji wa abiria na mazao ya chakula na biashara ziweze kuendelea.
Meneja wa Wakala ya Barabara (TANROADS) Mkoa wa Lindi, Mhandisi Emil Zengo, amesema kwa sasa eneo hilo limekamilika na barabara ya kutoka Liwale hadi Nangurukulu inapitika huku matengenezo madogo madogo katika baadhi ya maeneo yakiendelea kufanyika.
Baadhi ya wananchi wameonyesha kufurahishwa na kasi ya kurejeshwa kwa mawasiliano huku wakielezea adha waliyokuwa wakiipata awali ikiwemo kukosa mahitaji muhimu na kukwama kwa shughuli za kiuchumi.
Kwa upande wake Msimamizi wa barabara ya Kilwa Masoko-Nangurukuru-Liwale, Mhandisi Anna Nnko amesema mbali na daraja hilo, pia ipo sehemu ya barabara hiyo ilimegwa na maji, jambo ambalo lilifanya TANROADS kulazimika kuihamishia upande mwingine ili shughuli za kiuchumi ziweze kuendelea.
