Back to top

MAZIWA YASIYO SALAMA NI HATARI KWA MLAJI-SILINDE

30 May 2023
Share

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. David Silinde ameonya kuwa matumizi ya maziwa yasiyo salama huhatarisha maisha ya mlaji kutokana na kutumika kama njia ya kusafirisha  magonjwa ya mifugo kwenda binadamu.

Mhe. Silinde amesema hayo kwenye sherehe za ufunguzi wa Maadhimisho ya kitaifa ya Wiki ya unywaji maziwa duniani iliyofanyika Mei 30, 2023 kwenye viwanja vya Chipukizi mkoani Tabora.

“Mwaka huu maadhimisho haya ya Wiki ya unywaji Maziwa kitaifa tumeyaelekeza kwenye kusisitiza matumizi ya maziwa salama kwa sababu kumekuwepo na magonjwa mengi sana yanayosababishwa na maziwa yasiyo salama, mfano ugonjwa wa kutupa mimba ambapo mtu akinywa maziwa yanayotokana na ng’ombe anayeumwa ugonjwa huo naye huanza kuathiriwa  na tatizo hilo hapo hapo” Ameongeza Mhe. Silinde.

Mhe. Slinde amewataka Wananchi wote waliopo karibu na mkoa wa Tabora kufika kwenye maonesho hayo ili wapate elimu ya kutosha kuhusu sheria namba 8 ya maziwa ambayo inaanisha kila kitu kuhusu maziwa salama.

“Lakini pia tunatambua moja ya changamoto nyingine kubwa inayowakabili watumiaji wengi wa maziwa ni uchakachuaji wa maziwa hayo, kwanza huo ni wizi kwa sababu mlaji anatoa pesa ilia pate maziwa bora sio yale yaliyoongezwa maji lakini pili tumewaelekeza Bodi ya Maziwa kuhakikisha wanafikisha elimu ya uuzaji wa maziwa bora kwa wasambazaji na wauzaji wote wa bidhaa hiyo na baada ya hapo wale ambao watashindwa kukubaliana na elimu hiyo  tutawachukulia hatua kupitia sheria yetu ya maziwa” Amesisitiza Mhe. Silinde.

Kwa upande wake Msajili wa Bodi ya Maziwa nchini Dkt. George Msalya ametoa rai kwa wadau wote waliopo kwenye mnyororo wa thamani wa maziwa kuzingatia sheria ili kuhakikisha mlaji anapata maziwa yaliyo salama.

“Maziwa ni chakula bora sana na kiburudisho poa kwa watu wa rika zote wakati wote hivyo ni lazima sisi kama wenye dhamana ya kusimamia usalama wa bidhaa hii tunatekeleza wajibu wetu katika kuhakikisha mlaji haathiriki kutokana na matumizi ya zao hili la mifugo” Amesema Dkt. Msalya.

Akizungumzia hali ya uzalishaji na matumizi ya maziwa kwa mkoa wa Tabora, Kaimu Mkuu wa Mkoa huo ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Nzega Mhe. Naitapwaki Tukai amesema kuwa mkoa huo ndio unaoongoza kwa wingi wa ng’ombe hapa nchini hali inayowafanya gharama za maziwa kuwa chini ukilinganisha na maeneo mengine.

“Kwetu sisi wamasai maziwa ni chakula na ndio maana wengi tuna afya njema hivyo nitoe rai kwa wananchi wa mkoa wa Tabora tutumie fursa hii ya upatikanaji wa maziwa mengi mkoani kwetu kuboresha afya zetu na uchumi wetu kwa ujumla” Ameongeza Mhe. Tukai

Maadhimisho hayo ya kitaifa ya Wiki ya unywaji maziwa huambatana na shughuli mbalimbali zinazolenga kuhamasisha matumizi ya maziwa na huanza Mei 29 ya kila mwaka na kufikia tamati Juni 1  ambapo kwa mwaka huu yanatarajiwa kuhitimishwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega.