Back to top

Mbio za Mwenge wa Uhuru zaahirishwa kujihami na Corona.

16 March 2020
Share

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameahirisha Mbio za Mwenge wa Uhuru za mwaka huu zilizopangwa kuzinduliwa tarehe 02 Aprili, 2020 huko Unguja, Zanzibar kwa lengo la kuchukua tahadhari ya kusambaa kwa virusi vya ugonjwa wa Corona (Covid-19) endapo utaingia hapa nchini.

Mhe. Rais Magufuli ametangaza maamuzi hayo leo asubuhi tarehe 16 Machi,2020 alipokuwa akiwasalimu wananchi wa Ubungo, Mbezi Mwisho na Kibamba Jijini Dar es Salaam, wakati akikagua maendeleo ya upanuzi wa barabara na ujenzi wa barabara za juu katika makutano ya barabara za Morogoro, Sam Nujoma na Mandela eneo la Ubungo (Ubungo Interchange).

Pamoja na kuahirisha Mbio za Mwenge wa Uhuru, Mhe. Rais Magufuli ameagiza fedha zilizoandaliwa kwa ajili ya mbio hizo zipelekwe Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa ajili ya maandalizi ya kujiweka tayari endapo ugonjwa wa Corona utaingia hapa nchini.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewasisitiza Watanzania wote kuendelea kuchukua tahadhari ya kuambukizwa virusi vya ugonjwa wa Corona kwa kuepuka misongamano, kutogusana, kunawa mikono kwa sabuni na maji yanayotiririka na kuzingatia maelekezo mengine ya wataalamu wa afya, lakini amesema ugonjwa huo bado haujaingia hapa nchini.