Back to top

WIZARA YA FEDHA HARAKISHENI FEDHA: WAZIRI MKUU

20 February 2026
Share

WIZARA YA FEDHA HARAKISHENI FEDHA: WAZIRI MKUU

#HABARI: Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mwigulu Nchemba ameitaka Wizara ya fedha kuharakisha upatikanaji wa fedha ili kuiwezesha Wizara ya Ujenzi kuanza ujenzi wa miradi ya barabara zilizosainiwa.

Amesema hayo wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro alipokagua barabara ya Holili Rotima- Tarakea Nayemi km 52.8 na kusisitiza ujenzi wake sehemu ya Ikuini -Kirongo Chini km 10 ijengwe  mara moja.

"Barabara hii ni muhimu kwa kuwa inapita maeneo ya mpakani, yenye uzalishaji wa mazao ya kilimo, itakuza biashara na huduma za utalii na kuongeza tija katika kituo cha forodha cha  Tanzania na Kenya "(Tarakea)," amesema Dkt. Nchemba.

Nae Naibu Waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey Kasekenya amesema Serikali imepanga kuijenga barabara yote ya HoliliRotima-Tarakea Nayemi km 52.8 kwa kiwango cha lami.

Amebainisha kuwa zoezi lililobaki ni kuwalipa wananchi 1,143 fidia ya zaidi ya shilingi  bilioni 14.6  waliopisha mradi huo.

Aidha,  Eng. Kasekenya amebainisha kuwa Serikali itaijenga barabara ya Elerai-Kamwanga km 40 ili kuziunganisha vizuri Wilaya za Rombo na Siha na kuuzunguka mlima Kilimanjaro kwa barabara ya lami na hivyo kuchochea ukuaji wa utalii mkoani humo. 

Waziri Mkuu Dkt. Nchemba anaendelea na ziara yake mkoani Kilimanjaro kukagua miradi ya maendeleo  na kuzungumza na wananchi.