Back to top

MIFUMO YA KIDIJITALI KWENYE KILIMO BIASHARA KUIMARISHWA

24 February 2026
Share

Tanzania na Uholanzi zimedhamiria kuimarisha ushirikiano kwenye matumizi ya mifumo ya Kidijitali kwenye huduma za Kilimo na Biashara za mazao na kujengea uwezo watumishi wanaosimamia mfumo wa Agricultural Trade Management Information System(ATMIS) unaoboreshwa kuwa mfumo wa e-Kilimo. 

Maazimio hayo yamejiri wakati Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli, alipokutana kwa mazungumzo na ujumbe kutoka Uholanzi uliongozwa na Bw. Lex Morret, mtaalam kutoka Mamlaka ya Usalama wa Chakula na Bidhaa za Watumiaji ya Uholanzi, katika Ofisi za Wizara ya Kilimo, Jijini Dodoma.

Bw. Lex ameeleza kuwa Serikali ya Uholanzi iko tayari kuisaidia Tanzania katika matumizi ya saini za kidigitali (Electronic Signature) kupitia Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Kiing. Southern African Development Community (SADC) pamoja na kuanzisha na kutumia mfumo wa e-phyto kwa mujibu wa miongozo ya Mkataba wa Kimataifa wa Ulinzi wa Mimea (International Plant Protection Convention - IPPC). 

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Mweli ameishukuru Serikali ya Uholanzi kwa utayari wake wa kuendelea kudumisha ushirikiano na Tanzania katika nyanja mbalimbali za kuleta maendeleo nchini ikiwemo Sekta ya Kilimo. Ameongeza kuwa Wizara ya Kilimo iko tayari kupokea ushirikiano huo ili kuimarisha mifumo ya kidijitali na biashara za mazao kwa manufaa ya wakulima na Taifa kwa jumla.