
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amesema Rais wa Tanzania Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan, anataka kuona ushiriki mkubwa zaidi wa Makandarasi wazawa katika kazi za utekelezaji wa ujenzi wa miradi nchini.
Waziri Bashungwa amebainisha hayo katika Mkutano wa mashauriano kati ya Serikali na Makandarasi wazawa na Washauri elekezi wa ndani Jijini Dodoma, kujadili nafasi yao katika utekelezaji wa miradi.
Bashungwa amesema Wizara ya Ujenzi, kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), inaendelea kutenga miradi mikubwa ya ujenzi wa barabara kwa ajili ya Makandarasi wa ndani kwa lengo la kuwasaidia Makandarasi hao kukua na kupata uzoefu.
Aidha, Bashungwa amesisitiza kuwa katika mwaka wa fedha 2023/2024 Jumla ya kilometa 20 za barabara zimetengwa kwa ajili ya makandarasi wanawake, ambapo zitagawanywa katika vipande vya kilometa tano tano, na kazi hizo zitashindanishwa kwa makampuni ya wanawake peke yao, hii inafanya jumla ya km 220 kujengwa na makandarasi wazawa kwa mwaka 2023/24.
Bashungwa ameongeza kuwa kazi za matengenezo ya barabara zinazosimamiwa na TANROADS kwa kutumia fedha za Mfuko wa Barabara zenye thamani ya Shilingi Bilioni 600 zitatekelezwa na Makandarasi wa ndani tu katika mikoa yote 26 nchini.
Halikadhalika, Bashungwa amefafanua kuwa Sheria ya Ununuzi wa Umma imefanyiwa marekebisho kwa kuongeza kiwango cha thamani ya mradi ambao utatekelezwa na Makandarasi wa ndani tu, bila kushindanishwa na Makandarasi wa nje.
Dhima kuu ya mkutano huu ni kujadili na kudadavua mikakati mbalimbali kati ya Serikali na wadau wa Sekta ya Ujenzi kuhusu kuwajengea uwezo makandarasi wazawa na washauri elekezi.