Back to top

MIPANGO YA KUPIMA VIWANJA IENDANE NA MIUNDOMBINU

06 October 2023
Share

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Jerry Silaa, amewaelekeza wataalamu wa sekta ya ardhi nchini kuhakikisha mipango yote ya kupima viwanja inaendane na miundombinu ya maeneo husika.

Silaa ametoa maagizo hayo Jijini Arusha wakati akizungumza na uongozi pamoja na watendaji wa sekta ya ardhi akiwa katika ziara yake ya siku moja mkoani Arudsha.

Amesema ili sentesi ya jina la Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ikamilike lazima wataalamu wanapopima viwanja basi viwanja hivyo viwe na uwezo wa kusaidia huduma za miundombinu kwenye nyumba iliyojengwa pamoja na makazi.

Kwa mujibu wa Waziri Silaa, suala hilo lazima liendane na aina ya uendelezaji au ujenzi ili mhusika afahamu kama kiwanja alichochukua atajenga nyumba ya aina gani kama ni ya chini ama ghorofa.

Akielezea zaidi kuhusu zoezi la kupanga, kupima na kumilikisha (KKK) Silaa amesema, katika kipindi hiki anachohudumu wizara ya ardhi mkazo wake mkubwa utakuwa kwa zile K mbili za Kupanga na Kupima ambapo amesisitiza kuwa, maeneo yote yanayoenda kupimwa ardhi basi wataalamu wasijifungue kama wataalamu wa fani moja na kuwaachia watu vichaka.