Back to top

Mkapa kuzikwa karibu na makaburi ya wazazi wake Lupaso, Mtwara.

29 July 2020
Share

LUPASO, MTWARA

Rais wa awamu ya Tatu Mhe.Benjamin Mkapa aliyefariki dunia juma lililopita jijini Dar es Salaam anazikwa leo kijijini kwake Lupaso,  wilayani Masasi mkoani Mtwara karibu na makaburi ya wazazi wake.

Mwili wa marehemu Mkapa uliwasili kijijini Lupaso jana ukitokea jijini Dar es Salaam baada ya kuagwa na maelfu ya wananchi na baadaye kuagwa kitaifa na viongozi mbalimbali walioongozwa na Rais Dkt.John Magufuli.

Kabla ya tukio hilo mwili ulipelekwa katika Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Theresa la Mtoto Yesu ambamo ilifanyika ibada ya Misa Takatifu ya kumuombea marehemu.

Akizungumza kabla ya kuuaga mwili kitaifa, Rais Dkt.Magufuli alisema msingi wa mafanikio ya kiuchumi yanayoshuhudiwa nchini Tanzania uliwekwa na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu marehemu Mkapa.

Alisema Taifa limempoteza kiongozi aliyetoa mchango mkubwa katika nyanja mbalimbali, kazi ambayo imeiwezesha kuifikisha Tanzania iilipo kiuchumi na maendeleo ya jamii.

Leo asubuhi kulifanyika ibada ya Misa takatifu katika Kanisa Katoliki la Lupaso kumuombea marehemu ambapo katika mahubiri yake, Askofu Mkuu wa Jimbo la Mbeya Mhashamu Gervas Nyaisonga ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania alisisitiza umuhimu wa wanadamu kuishi kwa upendo, umoja na kuyatenda mapenzi ya Mungu.

Watu binafsi na makundi mbalimbali yanaendelea kuomboleza kifo cha marehemu Benjamin Mkapa.