Back to top

Mkoa wa Katavi umekithiri kuwa na wahamiaji haramu wengi.

04 July 2020
Share

MPANDA.
_________

Waziri Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa amewataka watu wanaoishi kwenye makazi ya Mishamo na Katumba wawe waadilifu na wasitumike kama madalali wa kuingiza wahamiaji haramu nchini.

Amesema mkoa wa Katavi umekithiri kwa kuwa na wahamiaji haramu wengi, hivyo amemuagiza Mkuu wa Mkoa huo Bwana Juma Homera ashughulikie tatizo hilo.

Ametoa agizo alipozindua jengo la ofisi na biashara la Mpanda Plaza lililojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) mjini Mpanda kwa gharama ya shilingi bilioni mbili na milioni mia nane.

Waziri Mkuu amesema Katavi imetulia lakini haijatengamaa kwa sababu ni kati ya mikoa yenye idadi kubwa ya wahamiaji haramu nchini ambao njia yao wanayotumia kuingilia ni makazi ya Katumba na Mishamo.

Amesema Tanzania haijazuia watu wa mataifa mengine kuingia nchini, ila inawataka wafuate taratibu zilizowekwa na siyo kuingia kwa kutumia njia za panya.

Amesema ana majina ya watu zaidi elfu mbili walioingia Tanzania kwa njia za panya na wamejiingiza katika maeneo mbalimbali, hivyo amewataka warudi kwao na wafuate taratibu kabla ya kuja tena nchini.