
Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa Takukuru imempandisha kizimbani Mkurugenzi wa huduma na uwezeshaji wa taasisi ya uhasibu nchini Bw.Zodo Miraji kwa tuhuma za uhujumu uchumi na kusababisha hasara ya zadi ya Shilingi Milioni 147.
Shauri hilo lipo mbele ya Hakimu mkazi mkuu Mh. Thomas Simba ambapo mtuhumiwa anatetewa wakili Jamhuri Johnson.
Mwanasheria wa Takukuru Bw. Max Ali aliiambia Mahakama kuwa kati ya tarehe moja Mei mwaka 2014 na Mei Mosi mwaka 2016 mtuhumiwa akiwa ni Mkurugenzi huduma na uwezeshaji na akiwa mwajiriwa wa taasisi hiyo alishindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo na kuisababishia taasisi hasara.
Hata hivyo Mwanasheria huyo wa Takukuru aliiambia Mahakama kuwa upelelezi wa shauri hilo haujakamilia na kutokana na kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka Mahakama imepewa kibali ili kuruhusu Mahakama ya Kisutu kuweza kusikiliza shauri hilo.
Kufuatia kibali hicho hakimu simba ametoa dhamana kwa Masharti ya wadhamini wawili wanaoaminika na watakaosaini bondi ya Shilingi Milioni 73 pamoja na mtuhumiwa kusalimisha hati yake ya kusafiria na kutotoka nje ya Dar es Salaam bila ya kibali cha Mahakama.
Aidha wadhamini hao wawe na barua na vitambulisho vya ofisi zinazotambulika, hatua ambayo wadhamini wamekidhi vigezo na mtuhumiwa yupo nje na kesi hiyo itakuja tena aprili 16 mwaka huu.
Katika shauri lingine la kesi inayomkabili aliyekuwa muHasibu mkuu wa Takukuru Bw. Godfrey Gugai litafikishwa mbele ya Hakimu mkazi mkuu Simba tarehe 10.
Gugai pamoja na wenzake wawili wanakabliwa na mashtaka 43 yakiwemo ya utakatishaji fedha haramu, kumiliki mali zisizoendana na kipato na kughushi mikataba ya mauziano ya viwanja katika maeneo mbalimbali.