
Rais Dk.Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye mkutano wa Afrika wa kujadili uvuvi mdogo na wavuvi wadogo, utakaofanyika nchini mwezi ujao.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdalah Ulega, Jijini Dar es Salaam na kusema mkutano huo utafanyika kuanzia Juni 5 hadi 7 na kwamba utawakutanisha Mawaziri wa sekta ya uvuvi kutoka nchi za Afrika, kampuni za kikanda na kimataifa, asasi za kiraia, wafanyabiashara wakubwa, benki na wavuvi wadogo.
Amesema lengo la mkutano huo ni kubadilishana uzoefu, kujadili mbinu za kisasa za kuwasaidia wavuvi wadogo, namna ya kukabili uvuvi haramu na hatima ya uvuvi mdogo barani Afrika.

Amesema hapa nchini wavuvi wadogo wanachangia asilimia 95 ya uvuvi wote unaofanyika kila mwaka kuanzia baharini hadi kwenye maziwa na mabwawa.
Ulega amesema takwimu zinaonesha kwamba takribani Watanzania milioni sita wanategemea uvuvi mdogo, ambao unachangia asilimia 1.9 ya pato la taifa na kuiingizia nchi zaidi ya Shilingi bilioni 509 ya fedha za kigeni kila mwaka.
Amesema baada ya mkutano huo, Afrika itatoka na msimamo wake kuhusu namna ya kuwasaidia wavuvi wadogo, mbinu za kukabili uvuvi haramu na hatima ya wavuvi mdogo barani Afrika.
Waziri Ulega amesema takwimu za mwaka jana zinaonesha kwamba zaidi ya mazao ya majini ya Shilingi trilioni 3.4 yalivuliwa wakiwamo samaki wa maji baridi tani 479,976.6.
Kwa mujibu wa Waziri Ulega, baadhi ya wavuvi wadogo wanaoendesha shughuli zao katika Bahari ya Hindi, ziwa Victoria, Tanganyika, Nyasa, Rukwa na mabwawa ya Nyumba ya Mungu na Mtera watahudhuria mkutano huo.
