
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Alexander Mnyeti, amewataka wafugaji mkoani Katavi kuondokana na ufugaji holela licha ya kuwepo kwa maeneo ya kutosha ya malisho ya mifugo yao.
Mhe. Mnyeti ameyasema hayo, kwenye Maadhimisho ya Wiki ya Mwanakatavi yanayoendelea mkoani humo ambapo leo ilikuwa ni siku ya Mifugo, Uvuvi na Lishe huku yeye akiwa mgeni Rasmi kwenye siku hiyo.





"Wizara inatambua mkoa huu ni miongoni mwa mikoa yenye mpango mzuri wa maeneo ya malisho lakini una mifugo mingi ambayo haina tija jambo ambalo linahatarisha hata uwepo wa maeneo hayo siku za usoni hivyo ni lazima muanze kufuga kisasa ili muwe na mifugo michache mnayoweza kuihudumia na maeneo mengine yatumike kwenye shughuli nyingine za maendeleo" Ameongeza Mnyeti.
Amegusia hali duni ya Lishe mkoani humo licha ya wingi wa mazao ya Kilimo na Mifugo Mhe. Mnyeti amewataka wananchi kuhamasika kufuga samaki kupitia Ziwa Tanganyika na kwenye mabwawa ili kuongeza kiwango cha upatikanaji wa samaki.
"Samaki kama alivyo ni protini ya kutosha kabisa na mkoa huu mna fursa ya kupata protini ya nyama, maziwa na samaki kwa sababu mnapitiwa na Ziwa Tanganyika ambalo licha ya kuvuna samaki waliopo pia mna fursa ya kuwafuga ziwani humo au kwenye mabwawa" Amesisitiza Mhe. Mnyeti.
Aidha Mhe. Mnyeti amempongeza Msindikaji mkubwa wa maziwa mkoani humo Bw. Maliki Salum kwa kazi nzuri anayoifanya ya kununua maziwa kwa wajasiriamali waliopo mkoani humo ambapo amemtaka kuanza kufuga ng'ombe wa kisasa wa maziwa ili awe na uhakika wa upatikanaji wa maziwa ya kukidhi uwezo wa kiwanda chake.
"Nimeambiwa kiwanda chako kwa sasa kinasindika lita 200 za maziwa kwa siku ambayo kwa sasa unayapata kwa tabu wakati ukiwa na ng'ombe 2 tu wa kisasa wanaweza kukuzalishia kiasi hicho, njoo pale Wizarani tukupe ng'ombe hao kutoka kwenye shamba letu la Mabuki" Amesema Mhe. Mnyeti
Mhe. Mnyeti amehitimisha siku hiyo kwa kutembelea tamasha la nyama choma linaloendelea kwenye Maadhimisho hayo ambapo mbali na kupata fursa ya kushuhudia mitindo tofauti ya uchomaji wa nyama na samaki alipongeza hamasa ya mkoa huo kwa wachoma nyama wanaofanya shughuli hiyo huku wakitembeza kwenye matoroli maalum yanayowawezesha kufikisha huduma kwa wateja popote walipo.
