Back to top

MNYETI AITAKA SEKTA YA UMMA KUWA YA MFANO KWENYE NANENANE

05 August 2024
Share

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Alexander Manyeti amezitaka taasisi za Serikali zinazoshiriki kwenye Maonesho ya kimataifa ya wakulima (NaneNane) kuwa wabunifu na kuonesha bidhaa bora ili sekta binafsi waweze kujifunza kutoka kwao.

Mhe.Mnyeti ameyasema hayo kwenye viwanja vya Maonesho ya NaneNane mkoani Morogoro, mara baada ya kumaliza kutembelea mabanda yote ya umma na yale ya sekta binafsi ambapo alioneshwa kufurahishwa na juhudi zilizooneshwa na sekta hiyo.

"Nimeona jinsi ambavyo sekta binafsi wanaipenda nchi yao kwa sababu pamoja na kufanya kazi zao kibiashara wanatoa huduma kwa sehemu kubwa na tumeona namna wanavyowasaidia wafugaji, wavuvi na wakulima pembejeo za shughuli zao na kinachofurahisha zaidi viwanja vyote ni vya ndani" Ameongeza Mhe.Mnyeti.

Mhe.Mnyeti amesisitiza kazi ya Serikali ni kuonesha njia, kusimamia na kuonesha mwelekeo hivyo ni vizuri wawe mfano kwenye aina ya bidhaa wanazopeleka kwenye maonesho hayo.

Katika hatua nyingine Mhe.Mnyeti amekoshwa na aina ya teknolojia zilizooneshwa na wadau mbalimbali wanaoshiriki kwenye Maonesho hayo ambapo ametoa rai kwa wananchi kufika kwenye viwanja mbalimbali kunakofanyika maonesho hayo ili waweze kubadili mifumo yao ya kilimo, ufugaji na Uvuvi.