Back to top

Mnyeti kuinyang'anya halmashauri ya Mbulu mil 500.

14 July 2019
Share

Mkuu wa Mkoa wa Manyara Bwana Alexander Mnyeti amesema atazirejesha shilingi milioni 500 hazina kuu zilizotolewa kwa ajili ya kuanza ujenzi wa majengo ya halmashauri mapya ya mji wa Mbulu kutokana na baraza la madiwani kushindwa kuidhinisha ujenzi huo kwa takribani miaka minne sasa kutokana na minyukano ya wenyewe kwa wenyewe ya kisiasa inayokwamisha jitihada za serikali za kuwasogezea wananchi huduma za karibu.

Bwana Mnyeti ametoa kauli hiyo mbele ya Mkuu wa wilaya hiyo Bwana Chelestino Mofuga baada ya kutoridhishwa na hoja ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa hesabu zilizokaguliwa za mwaka 2017/18, kujirudia kila mwaka, huku akisema mamilioni hayo yanapaswa kurejeshwa hazina kuu ili kuifuta hoja hiyo isijirudie kwa kuwa upo mgomo baridi kwa madiwani na kuiacha halmashauri hiyo mpya kukosa majengo ya halmashauri waliyoomba.

Hata hivyo Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo ya mji wa Mbulu Bwana Valerian Gidishang amesema, ujenzi huo unakwamishwa na baadhi ya madiwani licha ya kupitisha kuanza kwa ujenzi, huku baadhi ya madiwani wakikiri kupitisha lakini wakipinga kiasi cha malipo ya fidia kwa mmiliki wa ardhi na misuguano ya kisiasa kwa baadhi ya wanasiasa.