Back to top

MPANGO KUKOMESHA UVUVI HARAMU WAJA

26 May 2023
Share

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amesema Serikali inaboresha mfumo wa utoaji wa vibali vya kuingiza zana za uvuvi nchini ili kudhibiti uingizwaji wa zana haramu ikiwemo nyavu zenye matundu madogo na makokoro.

Waziri Ulega alitoa kauli hiyo Bungeni jijini Dodoma, wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe.Aleksia Asia Kamguna aliyetaka kujua Serikali imejipangaje kukomesha uvuvi haramu wa kuvua samaki kwa kutumia nyavu zenye matundu madogo (Kokoro).

Amesema kuwa Wizara yake kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo Ofisi ya Rais TAMISEMI imeandaa Mkakati wa muda mfupi na muda mrefu wa kudhiti vitendo vya uvuvi haramu nchini.

"Utekelezaji wa mkakati huo utashirikisha viongozi wa ngazi za Vijiji, Kata, Tarafa, Wilaya na Mikoa ili kudhibiti matumizi ya zana haramu ikiwemo nyavu zenye matundu madogo, kokoro na nyinginezo"Amesema Ulega

Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kutoa elimu kwa wavuvi, waingizaji na wasambazaji wa zana za uvuvi pamoja na jamii kuhusu athari za matumizi ya zana haramu za uvuvi zikiwemo nyavu zenye matundu madogo, kokoro, timba, freemaya pamoja na matumizi ya vilipuzi katika uvuvi.

Aidha, amesema Serikali inaendelea kuimarisha shughuli za ukaguzi wa zana za uvuvi zinazoingizwa nchini kupitia njia za mipakani na bandarini kwa kuongeza idadi ya watumishi na vitendea kazi kitendo ambacho kitaongeza wigo wa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika maeneo ya mipakani na bandarini.