
Makamu Mwenyekiti wa bodi ya Taifa ya Msaada wa Kisheria Ndg.Saulo Prosper Malauri, amesema Kampeni ya Mama Samia Legal Aid, imesaidia kwa kiwango kikubwa kuwaleta pamoja Wadau mbalimbali, kuwahudumia Wananchi wenye shida ya msaada wa kisheria na kutatua migogoro ya masuala ya Ardhi, Ndoa, Mirathi, Utawala, Ukatili wa Kijinsia, Matunzo ya Watoto na kutoa elimu ya Masuala ya kisheria kwa jamii.
Malauri amesema Mama Samia Legal Aid Campaign, imesaidia kuongeza uelewa kwa jamii, kwa sababu kuna changamoto nyingi zinazotokana na watu kukosa haki zao sababu ya uelewa na kutokujua taratibu za kufuata pindi wanapokuwa na migogoro mbalimbali.
Ameyasema hayo Jijini Dar- es Salaam, baada ya kikao kati ya Waziri wa Katiba na Sheria Mhe.Pindi Chana na bodi ya Taifa ya Ushauri ya Msaada wa Kisheria, ambapo ameeleza kuwa ushahidi unaonesha kwenye ile Mikoa ambayo tayari timu ya kampeni imekwishapita watu wengi zaidi wamefikiwa kirahisi na migogoro mingi imeweza kusuluhishwa ndani ya muda mfupi.
Aidha Kampeni ya Mama Samia Legal Aid kwa sasa inaendeela katika Mkoa wa Singida mpaka tarehe 19 Januari 2024; mpaka sasa jumla ya Mikoa mitano ya Dodoma, Manyara, Shinyanga, Ruvuma na Simiyu ambapo jumla Halmashauri 35, Kata 397 na Vijiji/ Mitaa 1,046 imefikiwa katika utekelezaji wa Kampeni hiyo na Katika mikoa hiyo mitano, jumla ya wananchi 362,488 (Wanaume 179,874 wananwake 182,615 ) wamefikiwa kupitia elimu ya kisheria na huduma nyingine za kisheria.
