Back to top

MSALATO SATELLITE CITY KUWA MJI WA MFANO

24 August 2023
Share

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk.Angeline Mabula, amesema mradi wa Kupanga na Kupima na Kumilikisha Ardhi (KKK), eneo la Kitelela mkoani Dodoma, maarufu kama ‘Msalato Satelite City,’ utakuwa wa mfano kwa matumizi mbalimbali.

Akizungumza wakati wa uwasilisha taarifa ya wizara hiyo kuhusu mradi wa KKK, kwa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii,Jijini Dodoma, Dk Mabula amesema, mradi huo utahakikisha huduma mbalimbali zinapatikana katika eneo hilo sambamba na kuzuia ujenzi holela.

Wizara ya Ardhi inatekeleza mradi huo kwa kutwaa eneo katika mtaa wa Kitelela jijini Dodoma, lenye ukubwa wa takriban ekari 971; kisha kulipa fidia, kupanga na kupima eneo kwa ajili ya matumizi mbalimbali ambapo jumla ya viwanja 1,012 vimepimwa.

Kwa mujibu wa Dk Mabula, Wizara ya Ardhi kwa kushirikiana na Halmashauri ya Jiji la Dodoma katika utekelezaji ‘Mpango Kabambe’ wa jiji hilo, imekuwa ikitekeleza miradi mbalimbali katika Jiji la Dodoma.

"Suala la Kitelela, tunataka mradi huu uwe wa mfano, tunataka mradi usimamiwe na uwe tofauti na miradi mingine"amesema Dk Mabula.

Amebainisha kuwa, utekelezaji wa ‘Mpango Kabambe wa Jiji la Dodoma’ unaendana na malengo yaliyoainishwa kwenye ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), ya kupanga na kupima viwanja vipatavyo 2,500,000 kwa miaka mitano (2020-2025).

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wizara hiyo, Mhandisi Anthony Sanga, amesema kupitia mradi huo wa Kitelela, fedha zitakazopatikana zinatarajiwa kutumika kwa ajili kuanzisha miradi mipya kwenye maeneo mbalimbali nchini.

"Mradi wa Kitelela tunaufanya kama ‘demo’ na fedha zinazopatikana kupitia mradi huo zitumike kutwaa na kupima maeneo mengine, hii ni moja ya mikakati ambayo wizara inaendelea nayo" amesema Mhandisi Sanga.

Awali wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii waliipongeza wizara ya ardhi katika kutekeleza mradi wa kupanga, kupima na kumilikisha ardhi. Hata hivyo, wameitaka wizara hiyo kuhakikisha inadhibiti mapema ujenzi holela na kuacha kusubiri kufanya zoezi la urasimishaji makazi.

"Naipongeza Wizara kwa namna ilivyojipanga lakini ni vizuri ikawa pro- active hasa kwa ile miji inayokuwa na kuacha kusubiri kurasmisha makazi.‘’ alisema mjumbe wa Kamati Shaban Shekilindi ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Lushoto mkoa wa Tanga.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geofrey Pinda kwa upande wake alisema, wizara yake kwa sasa iko kazini na wajumbe wa kamati hiyo wanapaswa kuimani katika masuala mbalimbali inayotekeleza.