Back to top

Msingi wa Mafanikio ya kiuchumi Tanzania uliwekwa na Mkapa.

28 July 2020
Share

DAR ES SALAAM

Rais Dkt.John Magufuli amesema msingi wa mafanikio ya kiuchumi yanayoshuhudiwa nchini Tanzania umewekwa na aliyekuwa Rais wa awamu ya Tatu Benjamin William Mkapa.

Ametoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza wakati wa kuuaga kitaifa mwili wa aliyekuwa Rais wa awamu ya tatu Mhe.Mkapa kwenye uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Kabla ya kuagwa kitaifa, mwili wa Rais Mstaafu wa awamu ya tatu Mhe.Benjamin Mkapa ulipelekwa katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Imakulata, Upanga Jijini Dar es Salaam ambako wakati wa uhai wake alikuwa akisali, kwa ajili ya ibada ya kumuombea  ambapo kwa mujibu wa mwanafamilia ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Yohane Mbatizaji, Marehemu Mzee Mkapa aliomba atakapochukuliwa na Mungu Mwili wake upitishwe kanisani  hapo kwa ajili ya ibada.

Rais Magufuli alishindwa kuvumilia na kujikuta akibubujika machozi huku akisema Taifa limempoteza kiongozi aliyetoa mchango mkubwa katika nyanja mbalimbali, kazi ambayo imeiwezesha kuifikisha Tanzania ilipo kiuchumi na maendeleo ya jamii.

Ameyataja baadhi ya mambo ambayo kwayo Watanzania wataendelea kumkumbuka kuwa ni uanzishaji wa mipango ya kukuza uchumi ikiwemo kukuza biashara za wanyonge, MKURABITA, kukuza uchumi- MKUKUTA na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF.

Ameeleza marehemu Mkapa atakumbukwa kwa kuzifuta kodi mbalilbali zikiwemo kodi ya kichwa, kodi ya baiskeli na kodi ya mifugo, zilizokuwa zikiwasumbua wananchi na kusababisha wakati mwingine baadhi kulazimika kuzikimbia familia zao.

Rais Magufuli amesema katika sura ya kimataifa, Rais Mstaafu Benjamini Mkapa alikuwa Mwanadiplomasia mahiri na hata kufanywa kuwa mpatanishi wa migogoro mbalimbali na kujumuishwa katika taasisi mbalimbali za kimataifa.