Back to top

MUHIMBILI: MTOTO ATOLEWA SHANGA KWENYE MAPAFU

16 January 2024
Share

Madaktari Bingwa wa Upasuaji wa Kifua, Moyo, Mapafu na Mfumo wa Upumuaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, wamefanikiwa kuondoa shanga ya plastiki iliyokuwa imekwama katika pafu la kulia la mtoto mwenye umri wa miaka mitano baada ya kumpalia alipokuwa akiichezea mdomoni takribani mwezi mmoja uliopita.

Madaktari hao wamesema mtoto huyo alitaabika tangu wakati huo kwa kikohozi na kupumua kwa shida huku njia mbalimbali zikitumika kujaribu kuitoa na kugonga mwamba, ndipo wataalamu wa mapafu walipofanikiwa kuitoa bila madhara yoyote.
.
Madaktari hao wamesema walifanikiwa kutoa shanga hiyo kwa kutumia mpira laini wenye kamera ya video ya mapafu (Flexible bronchoscope) na kifaa cha kukamatia (foreign body basket), hivyo kumwepusha mtoto huyo na upasuaji mkubwa ambao ungesababisha ama kutoa pafu au sehemu ya pafu.

Kufuatia hali hiyo Jopo la madakatari walioshiriki kwenye zoezi hilo wamewaasa wazazi kufuatilia michezo ya watoto kwa karibu zaidi ili kuwazuia kuweka vitu mdomoni, puani pamoja na maskioni ili kuwaepusha na madhara mbalimbali ikiwemo madhara ya kudumu na kifo.