
Watalaam wa Magonjwa ya Mfumo wa Mapafu na Upumuaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, wamefanikiwa kutoa ganda la pipi kwenye pafu la kushoto la mwanamke mwenye umri wa miaka 53, kwa kutumia kifaa maalum chenye kamera kilichopelekwa moja kwa moja hadi lilipo na kulinasa, kisha kulitoa.
.
Akizungumza na vyombo vya habari baada ya kutoa ganda hilo, Daktari wa Magonjwa ya Mapafu na Mfumo wa Upumuaji, Dkt. Hedwiga Swai amesema kuwa mgonjwa huyo alifika hospitalini hapo, akiwa na tatizo la mapafu yake kuharibika na kutoa usaha vilevile alikua anatoa makohozi yenya harufu kali.
Dk.Swai ameeleza kuwa ganda hilo liliingia kwenye mapafu ya mgonjwa huyo, alipokuwa kimung'unya pipi na ganda lake mnamo mwaka 2013, kwa bahati mbaya akameza na ganda lake na alipoenda hospitali hawakuona tatizo lolote na kwamba baada ya muda alianza kukohoa na kutoa usaha, ndipo alipoanza kutumia dawa za kutibu ugonjwa wa Kifua Kikuu bila mafanikio yoyote.
.
“Mgonjwa huyo alikuja kwa lengo la kufanya vipimo vya kifua (Bronchoscopy) ila baada ya kuingiza kifaa chenye kamera kwenye mapafu tuliona kuna kitu ambacho sio cha kawaida katika pafu lake la kushoto na tulipoangalia vizuri tuligundua kuwa huo haukua uvimbe bali ni ganda la plastiki” alisema Dkt. Swai.
.
Kufuatia kisa hicho Dkt. Swai ameitaka jamii kuacha tabia ya kuchezea vitu mdomoni ambavyo vinaweza kuleta madhara kwakuwa kitu hicho kikingia kwenye mfumo wa hewa kinaweza kusababisha madhara makubwa.
