Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), kwa mara ya kwanza, imefanya upasuaji wa kutoa mfupa kwenye ubavu na kutengeneza kiungio (joint) cha taya la chini na fuvu ili kumtengenezea mgonjwa taya jipya la kulia lililoathiriwa na uvimbe.
.
Akizungumza baada ya upasuaji huo, Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Uso na Taya, Dkt. Arnold Augustino amesema, mgonjwa huyo amefanyiwa upasuaji wa kuondoa taya lote la kulia, lililoathiriwa na uvimbe na hivyo kumtengenezea taya jipya kwa kuchukua mfupa kutoka kwenye ubavu ambapo mfupa huo umepandikizwa kwenye kiungio cha taya, na kwamba mifupa mingine imechukuliwa kutoka kwenye nyonga pande zote mbili ili kuunganishwa na mfupa uliotolewa kwenye ubavu kuwezesha kutengenezwa kwa taya sawasawa na taya lake la awali na kisha kuunganishwa na kipandikizi cha chuma maalum kutengeneza sehemu ya taya iliyoharibika.
.
Amesema, mgonjwa huyo amefanyiwa upasuaji wa aina tatu tofauti kwa wakati mmoja, uliochukua saa saba, ukishirikisha wataalamu mbalimbali kwenye Hospitali hiyo, ambapo wa kwanza ulikuwa ni kutoa kipande cha mfupa kwenye ubavu, wa pili ni kutoa mifupa kwenye nyonga zote mbili na wa tatu ni kuondoa uvimbe.
.
Baada ya upasuaji huo, mgonjwa huyo anategemea kuendelea kula na kutafuna kama kawaida kwani atawekewa meno bandia kwenye mfupa wa taya aliotengenezewa.