Back to top

Mvua yakata mawasiliano ya barabara kwa baadhi ya maeneo mkoani Tanga

20 May 2018
Share

Mvua za masika zinazoendelea katika baadhi ya maeneo mkoani Tanga zimesababisha kukosekana kwa mawasiliano ya barabara inayounganisha mji wa Pongwe hadi katika vijiji vitatu vya wakulima na wafugaji hatua ambayo imewaathiri vibaya wakazi wa maeneo hayo wakiwemo wanafunzi kushindwa kwenda shule sanjari na kuzorota kwa shughuli za kiuchumi. 

Wakizungumza katika eneo la Takanini baada ya gari la wagonjwa kushindwa kufika katika  vitongoji ambavyo hakuna huduma zozote za afya baadhi ya wakazi wa eneo hilo wamesema mbali na mvua kuharibu barabara hiyo pia wachimbaji wa mchanga wanaopitisha magari makubwa wamechangia kuvunja baadhi ya madaraja na kusababisha kukosekana kwa mawasiliano.

Akifafanua zaidi kuhusu uharibifu wa barabara hiyo balozi wa nyumba kumi wa mtaa wa Takanini Said Sawa ameiomba serikali kudhibiti wachimbaji wa Mchanga ambao wamechangia kwa kiasi kikubwa kuharibu barabara hiyo ikiwa ni pamoja na kuvunja Madaraja yaliyojengwa kwa kutumia Makalavati ya Chuma kutokana na kusafirisha shehena kubwa ya Mchanga.

Kufuatia hatua hiyo baadhi ya wafugaji wanaofuga na kusafirisha maziwa katika kituo cha ukusanyaji bidhaa hiyo kilichopo tarafa ya Pongwe jijini Tanga wameiomba serikali kuingilia kati uharibifu wa barabara unaofanywa na wachimbaji Mchanga kwenye Migodi ili kusaidia kuokoa maisha ya wakazi wa maeneo hayo.