Back to top

MWAKILISHI MKAZI UNDP AANZA ZIARA YA SIKU NNE NCHINI

10 May 2024
Share

Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Bw. Shigeki Komatsubara, ameanza ziara ya siku nne (04) kutathmini utekelezaji wa Mradi wa Kupambana na Ujangili na Biashara Haramu ya Nyara (IWT), unaotekelezwa na  Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii.

Bw. Shigeki ameeleza kuridhishwa na utekelezaji wa Mradi wa IWT wenye lengo la kudhibiti ujangili lakini pia kama mbinu mojawapo ya kuendeleza uchumi wa kijani kwa maendeleo ya Taifa.

Bw.  Shigeki ameipongeza Tanzania kwa hatua yake ya kutenga eneo kubwa la ardhi  kwa ajili ya Uhifadhi lakini pia kama fursa muhimu ya kukuza uchumi wa kijani kwa ajili ya maendeleo  endelevu ya Taifa.

 Aidha, ameongeza kuwa kuwa UNDP iko tayari kufadhili utafiti ambao utasaidia kufahamu hali ya uhifadhi wa Wanyamapori pamoja na  njia nzuri ya  kusaidia ustawi wa pamoja kati ya jamii zinazoishi kuzunguka hifadhi hizo na wanyamapori.

Akiwasilisha taarifa ya utafiti uliofanywa na Taasisi ya Utafiti ya Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) Mkurugenzi wa Utafiti wa Taasisi hiyo Dkt. Julius Keyyu amezitaja baadhi ya shughuli ambazo zimetekelezwa na TAWIRI kwa ufadhili wa Mradi wa IWT kuwa ni pamoja na kufanya tathmini ya hali ya migongano baina ya Wanyamapori na binadamu ambayo imewezesha kuandaliwa kwa programu ya kupambana na wanyamapori wakali na waharibifu katika mfumo ikolojia wa Ruaha – Rungwa.

Katika hatua nyingine Mwakilishi mkazi wa UNDP ametembelea Shirika la Hifadhi za Taifa  (TANAPA) na kupata tathmini ya shughuli zilizotekelezwa na Shirika hilo kupitia mradi wa IWT ambapo ameeleza kuridhishwa na maelezo ya namna utekelezaji wa mradi huo ulivyofanyika.