Back to top

NAIBU WAZIRI KATIBA AHIMIZA TEHAMA SEKTA YA SHERIA

25 February 2026
Share

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Zainab Katimba, amefanya ziara ya kikazi katika Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia cha Mahakama ya Tanzania kilichopo Temeke, jijini Dar es Salaam.

Ziara hiyo imelenga utendaji kazi wa kituo hicho, ubora wa huduma zinazotolewa, pamoja na hatua zinazochukuliwa katika kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa haraka, kwa usawa na kwa kuzingatia utu.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mhe. Katimba amesema Serikali imejipanga kuendelea kuimarisha sekta ya sheria na haki kwa kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma. Ameeleza kuwa juhudi hizo zinajumuisha kuboresha matumizi ya TEHAMA, kuimarisha miundombinu ya mahakama, na kuweka mazingira rafiki yatakayorahisisha wananchi kupata haki kwa wakati.

“Dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kila mwananchi anapata haki bila vikwazo, kwa wakati na katika mazingira yanayozingatia weledi na utu,” amesema Mhe. Katimba.

Kwa upande wake, mmoja wa wananchi waliopata huduma katika kituo hicho, aliyejitambulisha kwa jina la Mchungaji Daud Mashimo, amepongeza ubora wa huduma zinazotolewa akieleza kuwa kituo hicho ni mfano wa kuigwa kutokana na uratibu mzuri na mazingira rafiki kwa wateja.

Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia cha Temeke kinajumuisha Mahakama ya Mwanzo, Mahakama ya Wilaya, Mahakama ya Watoto na Mahakama Kuu. Aidha, kituo hicho kinatoa huduma mbalimbali ikiwemo msaada wa kisheria, ushauri nasaha pamoja na uwepo wa chumba maalum cha kunyonyesha, hatua inayolenga kuhakikisha huduma zinawafikia wananchi wote kwa kuzingatia mahitaji maalum ya makundi tofauti katika jamii