Back to top

NAIBU WAZIRI PINDA AINGILIA KATI MGOGORO WA FIDIA KILWA.

24 March 2024
Share

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleio ya Makazi Mhe.Geophrey Pinda, ameingilia kati mgogoro wa wananchi kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa mkoa wa Lindi wanaodai maeneo yao kutwaliwa bila ya kulipwa fidia.

Hatua hiyo ya Mhe.Pinda inafuatia kupewa malalamiko na Juma Faki Mjaka mkazi wa Kilwa anayedai kutwaliwa eneo lake inapojengwa Bandari ya Kilwa pamoja na familia ya Mwinyimanga inayodai kunyanyaswa kudhulimiwa eneo lao Masoko Pwani wilayani Kilwa.

Naibu Waziri ametembelea eneo inapojengwa Bandari ya Kilwa kwa lengo la kujiridhisha madai ya Mjaka na baadaye kukutana na familia ya Mwinyimanga wakati alipokwenda kufungua mkutano wa wadau kuhusu uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi katika wilaya ya Kilwa.

Baada ya kutembelea eneo inapojengwa Bandari ya Kilwa na kupata maelezo ya mlalamikaji Bw. Mjaka Mhe.Pinda ameagiza kuudwa Tume maalum itakayohusisha vyombo mbalimbali ili kubaini ukweli wa malamiko ya mwananchi.

Kwa upande wa familia ya Mwinyimanga inayodai kunyanyaswa na kutwaliwa ardhi yao kwenye eneo la Pwani Masoko katika  halmashauri ya Kilwa, Naibu Waziri alitaka makubaliano yanayofikiwa baina ya wanaomiliki ardhi na wale wanaotaka kutwaa eneo kuzingatiwa.

Amesema, lengo la wizara yake ni kuondoa migogoro ya ardhi isiyo na sababu ya msingi hivyo asingependa kuona wananchi wakiendelea kulalamika kwa kudhulumiwa maeneo yao.

Kufuatia hali hiyo, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe, Pinda ameziagiza halmasauri zote nchini kujitayaarisha kabla ya kutwaa maeneo ya wananchi ili ziweze kulipa fidia kwa wananchi na kuondoa malalamiko.