Back to top

NHIF TOENI HUDUMA MPAKA NGAZI YA ZAHANATI

05 June 2023
Share

Serikali imeuelekeza Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kutoa huduma mpaka ngazi ya zahanati kwa vituo zilizokidhi vigezo vya kupewa huduma hiyo, ikiwemo kigezo cha kusajiliwa. 
.
Maelekezo hayo yametolewa na Naibu Waziri wa Afya Dkt.Godwin Mollel, wakati akijibu maswali Bungeni Jijini.
.
 
"Nawaagiza Bima ya afya wapitie nchi nzima wahakikishe vituo vyote ambavyo vimetimiza hivi vigezo, ikiwemo kigezo cha kusajiliwa viingizwe na kuanza kutoa huduma hiyo." Amesema Dkt. Mollel. 
.
Amesema,  katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora katika vituo vyote vya kutolea huduma, tayari Serikali kupitia Wizara ya Afya imeagiza vifaa na vifaa tiba ambavyo vitasambazwa katika vituo mbalimbali nchini.
.
Sambamba na hilo Dkt. Mollel amesema, katika kuongeza huduma za dawa zinazotolewa na bima katika zahanati na vituo vya afya Wizara imeongeza idadi ya dawa, vifaa na vifaa tiba ngazi ya Zahanati kutoka aina 254 mwaka 2015 hadi kufikia aina 451 mwaka 2023.
.
Ameendelea kusema kuwa, idadi ya dawa, vifaa na vifaa tiba ngazi ya Kituo cha Afya kutoka aina 414 mwaka 2015 hadi kufikia aina 828 mwaka 2023  huku akisisitiza dawa zilizoongezeka zipo katika miongozo ya Serikali na hivyo hulipiwa na Bima ya Afya kwa wanufaika wa mfuko. 
.
Sambamba na hilo, Dkt. Mollel amesema katika kuhakikisha changamoto ya upatikanaji wa dawa za kisukari na shinikizo la damu inatatuliwa, Serikali kupitia Wizara ya Afya imeongeza bajeti ya ununuzi wa dawa utaosaidia kusambaza dawa hizo nchi nzima mpaka katika ngazi ya zahanati.