Back to top

"NISHATI JADIDIFU KUCHOCHEA UWEKEZAJI"-Mhandisi Luoga

08 June 2024
Share

Wizara ya Nishati imeshiriki Kongamano la Kitaifa la Nishati Jadidifu kwa mafanikio ambapo imetumia kongamano hilo kueleza juhudi zinazofanywa na Serikali katika uendelezaji wa Nishati Jadidifu nchini na hii ikijumuisha utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Nishati Safi ya Kupikia.

Akifungua kongamano hilo katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNCC) Jijini Dar es Salaam, Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga amesema Serikali inajiandaa kuzindua Mkakati na Mpango Kazi wa Kitaifa wa Nishati Jadidifu ili kuchochea uwekezaji mkubwa katika Nishati Jadidifu.

Amesema uzinduzi wa mkakati huo utaakisi vyema Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025, Malengo ya Maendeleo Endelevu ya mwaka 2015 na makubaliano mengine ya kimataifa na kitaifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi. 

Amesema Serikali pia inaandaa "Mkakati na Mpango Kazi wa Ufanisi wa Nishati Tanzania” utakaosaidia utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Nishati na malengo ya kimkakati ya kupunguza kasi ya nishati chafu  kwa asilimia 20 ifikapo mwaka 2025 huku lengo la jumla likiwa ni kuhakikisha upatikanaji wa huduma za gharama nafuu na za uhakika za nishati endelevu na ya kisasa kwa  wote.

Mha.Inocent Luoga aliwashukuru wafadhili mbalimbali waliowezesha Wiki hiyo kufanyika ikiwemo kampuni ya Sunking,  Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDP);  TANESCO, Ensol Tanzania Limited, Global Off- Grid Lighting Association (GOGLA); Africa Enterprise Challenge Fund (AECF) na Umoja wa Ulaya (EU).

Naye Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Wadau wa Nishati Jadidifu Tanzania (TAREA) Mha. Mathew Matimbwi, ameiomba Wizara ya Nishati kuwa  mwakilishi kutoka sekta binafsi awepo kwenye  Bodi ya REA ili kuimarisha utekelezaji wa masuala mbalimbali kuhusu nishati jadidifu.

Kaulimbiu ya Kongamano hilo ni "Nishati Mbadala kwa Uchumi Shirikishi na Kijani"