
Timu ya Nyabiyonza FC imeibuka mabingwa kwa mara ya tatu mfululizo katika mashindano ya mpira wa Miguu ya BASHUNGWA KARAGWE CUP 2024 yaliyoanza mwezi Julai 2024 na kufikia tamati Agosti 25, 2024 baada ya kuifunga timu ya Ndama kwa goli 2-1 Katika Wilayani Karagwe Mkoani Kagera.
Mashindano hayo yaliyoandaliwa na Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa (MB) yalizikutanisha timu 23 kutoka kila Kata za Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe, ambapo Sherehe za Fainali zilitanguliwa na mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu kati ya timu ya Nyakakika na Kihanga, ambapo timu ya Kihanga iliibuka kidedea kwa ushindi wa goli 3-0.
Akizungumza wakati akihitimisha michuano hiyo Mh.Bashungwa ameahidi kuendelea kuboresha Mashindano yajayo ili kuwa na chachu zaidi na kuleta mafanikio kwa kuwa lengo la mashindano hayo ni kuimarisha afya kwa vijana, kusaka vipaji na kuviendeleza kwa kuunda timu ya Halmashauri itakayoshiriki katika ligi mbalimbali ndani na nje ya Wilaya ya Karagwe.
Naye, Mratibu wa Ligi ya Bashungwa Karagwe Cup, Johnson Majara ameeeleza kuwa mashindano ya Bashungwa Karagwe Cup 2024 ni muendelezo wa mashindano yaliyoanza tangu mwaka 2017 ambapo kwa mwaka 2024 yalishirikisha timu kutoka kata 23 za Wilaya ya Karagwe zilizopangwa katika makundi sita (6) na mpaka kufikia mchezo wa fainali ni michezo 94 iliyochezwa katika ligi hiyo.
