Back to top

Nyumba zaidi ya 10 zachomwa moto wilayani Hanan’g mkoani Manyara.

01 August 2021
Share

Wakazi wa kijiji cha Waama wilayani Hanan’g mkoani Manyara wameiomba serikali kuingilia kati mgogoro wa mipaka kati yao na kijiji jirani cha Dirma kufuatia baadhi ya wavamizi kuvamia na kuchoma nyumba zao na kuteketeza baadhi ya mashamba ambapo wamedai kuwa mgogoro huo unahatarisha hali ya usalama katika maeneo yao huku baadhi ya familia zikikosa maeneo ya kuishi baada ya nyumba zao kuchomwa moto.

ITV imefika katika kijiji cha Waama na kushuhudia nyumba zaidi ya kumi zikiwa zimechomwa moto nyingine zikiwa zimebomolewa ambapo wakazi hao wamepaza kilio chao wakibainisha kuwa kwa sasa hawana mahala pa kuishi pamoja na familia zao.

Licha ya nyumba zao kuchomwa moto wakazi hao wameiomba serikali kufanya uchunguzi na kuwachukulia hatua watakaobainika kuhusika na vitendo hivyo kwani hata mazao yaliyokuwa yanakaribia kuvunwa mashambani yamechomwa moto.

ITV imemtafuta Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Waama Bw.Martin Gurtu ambapo amethibitisha kutokea kwa matukio hayo ambapo ameeleza hatua zinazoendelea kuchukuliwa na serikali kuanzia ngazi ya kijiji hadi wilaya.