Back to top

PINDA ATAKA USHIRIKIANO UWEKAJI MIPANGO YA MATUMIZI YA ARDHI

23 April 2024
Share

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe.Geofrey Mizengo Pinda, amesema Wizara yake iko tayari kutoa ushirikiano kwa Taasisi Nyingine za Serikali, ikiwemo Wizara za Kisekta kuweka mipango ya matumizi bora ya ardhi ikiwa ni hatua muhimu ya kukabiliana na migogoro ya Ardhi inayotokana na jamii za vijijini kuvamia maeneo ya Taasisi hizo. 

Akitolea mfano ushoroba wa Wanyama ulioko jirani na kiwanda cha Mbolea Minjingu unaozingunisha Mbuga ya Wanyama Tarangire na Mbuga ya Manyara Naibu Waziri Pinda amesema Wizara yake kupitia Tume ya Taifa ya Matumizi ya Ardhi pamoja na Wizara ya Mali Asili na Utalii hazina budi  kushirikiana kupima na kuweka mipaka ya ushoroba huo ambao uko hatarini kutoweka kutokana na shughuli za binadamu zinazoendelea jirani na eneo hilo.

Naibu Waziri Pinda amesema hayo wakati wa hotuba ya ufunguziwa Kikao cha Wadau na Tume ya Taifa ya Matumizi ya ardhi alipomwakilisha Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Jerry Silaa kufungua Mkutano huo Jijini Dodoma. 

Aidha, ameitaka Tume ya Taifa ya Matumizi ya Ardhi kushirikiana na Wizara ya Mali Asili na Utalii kuchukua hatua za haraka na mapema ili baadae isije kulazimika kutumia nguvu kuondoa watu katika eneo la ushoroba wa wanayama hao.

Katika hatua nyingine Waziri Pinda amezitaka mamlaka za upangaji nchini ambazizo ni Halmashauri zote nchini kuhakikisha mipango yote iliyoandaliwa  kwa kushirikiana na wadau inawasilishwa Tume ya Taifa ya Matumizi ya Ardhi ili ziweze kusajiliwa ili ziweze kupatiwa na kutangazwa katika Gazeti la Serikali. 

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Eng. Anthony Sanga amewambia wajumbe wa Kikao Kazi hicho kuwa Idadi ya Watu katika Vijiji imekuwa kiongezeka kwa watani wa asilimia 2.4 kwa mwaka akibainisha kuwa vijijini kuna kaya zaidi ya Mil.8.6 sawa na asilimia 60.3 ya Kaya zote Nchini. 

Kufuatia hali hiyo Eng.Sanga alisema Ardhi hiyo ikipangwa, kupimwa na kumilikishwa itakuwa inachangia maendeleo ya kiuchumi ikiwemo usalama wa chakula  na mtaji muhimu katika kuondoa umasikini hapa Nchini. 

Wakati huo huo Mkurugenzi wa Tume ya Matumizi Bora ya Ardhi Prof. Wakuru Magigi alibainisha kuwa ifikapo Juni mwaka huu Mipango yote ya Upangaji Vijiji Nchini itakuwa jumla ya  Mipango 3,993 ambayo inatekeleza na Mradi wa Uboreshaji Milki Nchini na Tume ya Taifa ya Matumizi ya Ardhi.