
Watanzania wametakiwa kuhakikisha wanakuwa na mipango bora ya matumizi ya ardhi kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo, kwani ardhi iliyopo haiongezeki na idadi ya watu inazidi kuongezeka.
.
Rai hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Geophrey Pinda, wakati akiwahutubia wananchi wa Jimbo lake la Kavuu, lililopo katika Halmashauri ya Mbimbwe, mkoani Katavi, ambapo amewaeleza kuwa Jimbo hilo kwa sasa limepiga hatua kubwa ya kimaendeleo ikilinganishwa na miaka ya nyuma.
.
Mkutano huo ambao pia umehudhuriwa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa na Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda, Naibu Waziri huyo wa Ardhi alisema, wakati serikali ikiandaa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, Watanzania wanatakiwa kuwa na mpango wa matumizi ya ardhi huku wakielewa changamoto kubwa iliyo mbele yao ni kuwa ardhi haiongezeki.
.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mpimbwe Shamimu Mwariko aliwapa ushauri wananchi wa Mpimbwe kuwa, kama wanataka halmashauri yao ifanane kimaendeleo na halmashauri zilizopiga hatua kubwa kimaendeleo basi wahakikishe wanawashika viongozi wanaofanya maamuzi ya kimkakati.
.
Naye Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa na Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Mizengo Pinda amemtaka Mbunge wa Jimbo la Kavuu ambaye ni mdogo wake kuwa karibu na wananchi wakati wote wa juhudi mbalimbali za kuliletea maendeleo jimbo lake.
.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda yuko jimboni kwake katika Halmashauri ya Mbimbwe mkoa wa Katavi kujumuika wananchi wa jimbo la Kavuu pamoja na mambo mengine kusheherekea Siku Kuu ya Chrismas na wananchi wa jimbo lake.
